Jumanne, 12 Novemba 2013

DCI Manumba astaafu Polisi, Mungulu amrithi

http://tanzanianewz.blogspot.com
 Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba amestaafu rasmi utumishi wa umma baada ya kufikia umri wa kustaafu kisheria wa miaka 60.
Manumba aliyeanza kulitumikia Jeshi la Polisi miaka ya 1970, nafasi yake itashikwa kwa muda na Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini (CID), Kamishna Isaya Mungulu.
“Wakati utaratibu wa uteuzi wa Mkurugenzi wa Upelelezi ukiendelea, Kamishna Mungulu, atakaimu nafasi hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa ya Polisi kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Msemaji wake, Advera Senso.
Akizungumzia kustaafu huko, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, amemshukuru na kumpongeza Manumba kwa weledi na uaminifu mkubwa aliouonyesha wakati wote alipokuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi.
Amemtaka aendelee kuwa msaada kwa jeshi hilo kwa kutoa ushirikiano wa namna yoyote ile unaoweza kusaidia kupunguza uhalifu nchini akisema usalama ni taaluma kama zilivyo nyingine.
Historia yake kikazi
Katika utumishi wake, DCI Manumba amelitumikia jeshi hilo katika nyadhifa mbalimbali zikiwamo katika Chumba cha Kupokea Mashtaka kati ya mwaka 1976 hadi 1977 na baadaye Mwendesha Mashtaka Wilaya ya Kibondo na Kasulu mkoani Kigoma kati ya 1977 na 1984.
Alikuwa Mkufunzi katika Chuo cha Polisi kilichopo Kurasini Dar es Salaam, kati ya mwaka 1984 na 1987 kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi ya Magomeni na Kinondoni. Manumba baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia 1987 hadi 1993.
Kati ya mwaka 1993 na 1995, alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi kati ya 1995 na 1996.
Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Kukabiliana na Uhalifu wa Kughushi Makao Makuu ya Upelelezi mwaka 1996 na 1997 na baadaye kuwa Mkuu wa Kitengo cha Usalama, Intelijensia na Kupambana na Biashara ya Dawa za Kulevya kwenye Makao Makuu ya Upelelezi kuanzia 1997 hadi 2001.
Mwaka 2001 hadi 2006 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na kuanzia mwaka 2006 hadi anastaafu, alikuwa Mkurugenzi wa idara hiyo.
Mapema Januari, jina la DCI Manumba lilitawala vyombo vya habari baada ya hali yake kuwa mbaya na kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni