SUMAYE-"NINASINGIZIWA UMASKINI"

Atumia Biblia kuonya, kukemea rushwa na ufisadi
Awataka viongozi wa kiroho waombee chaguzi za 2014/2015
Waziri Mkuu mstaafu katika serikali ya awamu ya tatu, Frederick
Sumaye, amesema wapinzani wake kisiasa ‘wanampakazia’ kuwa ni masikini
wa kutupwa, hivyo kukosa uwezo wa kuwapa fedha wanaomuunga mkono.
Alisema kauli hiyo inatolewa na wanasiasa wanaopinga jitihada zake
za kupinga rushwa, ufisadi na aina nyingine za uovu kwa jamii ya
Watanzania.
Sumaye, aliyasema hayo jana, alipokuwa akizungumza kwenye harambee
ya kuchangia shughuli za ujenzi katika Kanisa Katoliki, parokia ya
Mawella iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro na hotuba yake kupatikana kwa
njia ya mtandao jijini Dar es Salaam.
Alitoa mfano akisema, “kuna kiongozi mwanasiasa (hakumtaja jina)
aliwakuta watu wanaoniunga mkono wakinijadili, akawaambia huyo Sumaye ni
maskini atawapa nini? Jiungeni na kambi ya fulani atawapeni fedha
nyingi na shida zenu zitaisha.”
Kwa mujibu wa Sumaye, mwanasiasa kiongozi huyo alisema umasikini si sifa ya kuwa Rais wa nchi.
Alielezea kusikitishwa na kauli hiyo kwa vile hajawahi kutangaza azma ya kuwania urais wa Tanzania.
“Pili, mimi sio masikini ila ni kweli sina fedha za kuwanunua
wapiga kura wala utaratibu wa kuwanunua siutaki, kwa maana ni rushwa,”
alisema.
Alisema si sahihi kuitwa masikini kwa sababu alikuwa Naibu Waziri
na Waziri kamili kwa karibu miaka tisa, na hatimaye Waziri Mkuu kwa
miaka 10 bila kufukuzwa kazi, hivyo hayumo katika kundi la masikini.
ATUMIA BIBLIA KUKEMEA RUSHWA
Sumaye, alilazimika kutumia vifungu mbalimbali vya Biblia kuonya na
kukemea rushwa na ufisadi, huku akiwahamasisha viongozi wa kiroho
kushiriki kudhibiti vitendo hivyo.
Alisema katika utaratibu wa demokrasia, wapiga kura wanawachagua
viongozi kutokana na sifa nzuri za uongozi kama vile ushupavu, uaminifu
na uadilifu.
“Kama ilivyokuwa huko, zamani mtu anayetakiwa kuwa kiongozi anatafutwa na jamii na siyo yeye kusaka uongozi,” alisema.
Aliongeza, “mbaya zaidi ni pale msaka uongozi atakapotafuta nafasi
hiyo kwa njia zisizofaa kama vile rushwa na kuwanunua wapiga kura
nakadhalika.”
Alisema, utaratibu wa kuwekwa au kuchaguliwa katika nafasi bila
vishawishi vya rushwa, uliotumika tangu enzi za kale, ndio unaotakiwa
kutumika hadi leo.
Alisema kiongozi anapaswa kupatikana si kutokana nakuutafuta
uongozi kwa udi na uvumba wala kwa rushwa, bali kuibuliwa katikati ya
jamii husika, kutokana na ubora wa kiongozi na si vishawishi vyake.
Alisema chaguzi za Tanzania zimegubikwa na rushwa na vishawishi, badala ya ubora, uhodari ama tabia nzuri ya anayetaka uongozi.
KUHALALISHA RUSHWA
Kwa mujibu wa Sumaye, hivi sasa rushwa na matumizi makubwa ya fedha
za kuwanunua wapiga kura, vinataka kuwa utaratibu halali wa kuwapata
viongozi wa kuanzia vijijini hadi Urais.
Alinukuu Biblia katika kitabu cha Kutoka 23:8, inasema, “nawe
usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na
kuyapotoa maneno ya wenye haki.”
Alisema wanaotakiwa kuona ni viongozi wetu kwa sababu kuongoza ni kuonyesha njia.
“Kama sote tunaamini Biblia Takatifu na inasema rushwa hupofusha
macho hao waonao, na wewe na mimi tukamchagua kiongozi mla rushwa, au
mtoa rushwa au anayewanunua wapiga kura, hivi huyo kweli atatuongoza
tukafike tunakotaka kufika,” alihoji.
Alisema wakati Tanzania ikielekea kipindi cha chaguzi za 2014 na
2015, taifa linahitaji kuwapata watu wa aina ya Musa na Haruni na Joshua
wanaotajwa kwenye biblia ili Watanzania wafike Kanaani ya maendeleo
yao.
Alisema ikiwa taratibu sahihi za kuwapata viongozi zitakiukwa,
badala yake wapiga kura wakanunuliwa kwa rushwa, taifa litawapata
viongozi waliopofuliwa kwa utoaji au upokeaji wa rushwa.
Alisema hivi sasa matendo yanaongezeka kwenye baadhi ya sehemu,
yakifanywa na wanaoziwania nafasi hasa za juu za uongozi wa nchi.
Sumaye, alisema inaelekea fedha zinazotumika ni nyingi, zikiwa na
ishara ya kupatikana katika utaratibu wa rushwa na kufisadi mali za
nchi.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa juhudi anazofanya kupambana na rushwa hasa nyakati za chaguzi.
Alisema, wapinga rushwa na aina nyingine za ufisadi wanakabiliwa na ‘mashambulizi’ kutoka kwa wanaonufaika na uovu huo.
“Ukikemea tu rushwa basi utapachikwa sababu nyingi zisizohusika
ikiwemo ya kugombea urais mwaka 2015. Nasema katika hili, suala la
kugombea au kutogombea urais mwaka si sababu. Vita vyangu dhidi ya
rushwa siyo vya leo,” alisema.
TUSIMSINGIZIE MUNGU
Sumaye alisema mwaka ujao ni muhimu kwa mustakabali wa taifa, kwa
sababu kuna uchaguzi katika ngazi za serikali za mitaa na maandalizi kwa
Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Ni kweli viongozi huteuliwa na Mungu, lakini Mungu hufanikisha tu
hilo kama tutamtegemea yeye na kufanya yale yanayopasa kufanya.”
Naye Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM) Dk. Cyril Chami, alisema yeye si miongoni mwa viongozi wa kisiasa wanaotajwa (na Sumaye).
Chami ambaye amewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika
vipindi vyote vya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, aliyasema hayo muda
mfupi baada ya Sumaye kuzungumza.
“Mpigieni makofi mheshimiwa Sumaye kwa sababu yeye alikuwa
shahidi wakati huo ingawa sijui ahadi yangu au nitakachokitoa hapa sasa
hivi kitatafsiriwa kwamba ni rushwa au nitakuwa nimetimiza wajibu wangu
kama kiongozi…Lakini pia niseme mimi nilitafutwa na wazee wanne wa jimbo hili na wakaniomba nigombee, nikakubali.
Awali, Paroko wa Parokia ya Mawela, Padri Anthony Marunda,
akihubiri kanisani hapo aliwaonya watanzania kuepuka tamaa ya madaraka
huku akiwataka kujifunza masuala ya uongozi wa nchi kutoka kwa mfalme
Herode anayetajwa katika Biblia kwamba alikuwa mpambanaji asiyekatishwa
tamaa na watawala.
Kuhusu hafla ya uchangiaji ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa kanisa
hilo ambao utagharimu zaidi ya Sh milioni 450, utakuwa na uwezo wa
kuhudumia watu 504 kwa wakati mmoja ukiwa na vifaa maalumu vya kutafsiri
lugha na kamera za usalama ambazo zitasaidia kuepusha baadhi ya maafa
ikiwemo uhalifu wa kimtandao. Ahadi zilizopatikana ni Sh. milioni 170 na
fedha taslimu Sh. milioni 55.2.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni