Kilimanjaro Stars na Uganda the Cranes Kufungua mechi za robo fainali Cecafa leo

ROBO Fainali za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, Cecafa Chalenge zinatarajiwa kuchezwa leo Uwanja wa Manispaa, Mombasa, Kenya.
Mchezo unaotarajiwa kuvuta na kuteka hisia za watu wengi ni kati ya mabingwa watetezi, Uganda The Cranes dhidi ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars itakayoanza kuchezwa saa 8:00 mchana, na kufuatiwa mechi nyingine kati ya Kenya na Rwanda saa 10:00 jioni.

Kilimanjaro Stars wanaingia kukutana na The Cranes inayofundishwa
na kocha Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’,kwenye kumbukumbu Timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars yenye idadi kubwa ya wachezaji wa Bara
ilifungwa nyumbani na ugenini na Uganda katika mechi za kuwania tiketi
ya kucheza Fainali za CHAN.
Kwa Uganda inaonyesha kuwa mbali zaidi hasa katika Challenge ya
mwaka huu baada ya kufuzu Robo Fainali kwa kushinda mechi zake zote za
Kundi C, wakati Kilimanjaro Stars ilipata ushindi wa goli 1-0 mara
mbili na sare moja hivyo kushika nafasi ya pili Kundi B.
Kocha Mdenmark, Kim Poulsen amesema kwamba anawaheshimu Uganda ni
timu nzuri na anatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini yeye amewaandaa
vyema vijana wake kushinda mechi ya leo.
Micho pia amesema Stars ni wazuri hasa baada ya kuwasili kwa
washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu
ambao amesema wakiungana na Mrisho Ngassa watetengeneza safu kali ya
ushambuliaji.
Kwa ujumla makocha wote wanaogopana kwenye mchezo huu wa leo jambo
ambalo linaashiria mechi hii kuwa kali na isiyotabirika hata chembe.
Safu ya ushambuliaji ya Stars leo inatarajiwa kuongozwa na Ngassa,
Ulimwengu na Samatta wakati viungo wanaweza kuwa Frank Domayo, Salum
Abubakar ‘Sure Boy’ na Athumani Iddi ‘Chuji’.
Langoni atakua ni Ivo Mapunda, kulia Himid Mao, kushoto Erasto Nyoni na katikati Said Morad na Kevin Yondan.
Kwa upande wa mabingwa watetezi, Uganda, Emanuel Okwi, Hamisi Kiiza
na Dani Sserunkuma wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji, wakati
wengine kikosini watakuwa Nico Wadada, Godfrey Kizito, Khalid Aucho,
Brian Majwega, Vincent Kayizzi, Godfrey Walusimbi, Savio Kabugo na
Benjamin Ochan langoni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni